UTOTO MTAKATIFU

MKURUGENZI: Fr. Lucas MGAYA

MLEZI: Sr. Lucia MPETE OSB

UTANGULIZI

Shirika la Utoto Mtakatifu kama sehemu ya Shirika la Kipapa la uenezaji injili.

Shirika kuu la kueneza injili kwa mataifa chini ya uongozi na mamlaka ya Baba Mtakatifu linaitwa kwa lugha ya kingereza: “Sacred Congregation for the Evangelisation of peoples” au kwa kilatini “Sacra Congregatio pro Evangelisatione Gentium” kwa kifupi “Propaganda Fide”. Wajibu na jukumu la shirika hilo ni kuongoza, kusimamia na kuratibisha kazi za kueneza injili kote ulimwenguni – hasa katika nchi za misioni.

Shirika hili husimamiwa na Kardinali aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu mwenyewe ili kufanya kazi kwa niaba yake. Kwa sasa, Kardinali msimamizi wa shirika hilo ni Mwadhama Josef Kardinali Tomko, Mzaliwa wa Yugoslavia.

Kufuatana na mwongozo wa hilo Shirika kuu la kueneza injili, yaliundwa kwa nyakati mbalimbali mashirika madogo manne ndani na chini ya Shirika Mama katika kazi ya kueneza Injili Ulimwenguni kwa njia ya sala, sadaka na michango mbalimbali ya hali na mali.

Kama lilivyo Shirika Mama, hali kadhalika mashirika hayo manne yanayo hadhi ya kipapa; ndiyo kusema kuwa Baba Mtakatifu ni Mkuu na Msimamizi Mkuu wa mashirika hayo.

Mashirika hayo yanaweza kuorodheshwa kama ifuatavyo:

  • Umoja wa Kimisionari wa Mapadre (Missionary Union of Clergy)
  • Shirika la kueneza imani (Society for the Propagation of the faith)
  • Shirika la Mtakatifu Petro Mtume la Kuwalea Mapadre Wazalendo (Society of St. Peter the Apostle for the Diocesan Clergy).

Shirika la Utoto Mtakatifu au Shirika la Mtoto Yesu (Society of the Holy Childhood).

Kama lilivyo Shirika Mama, mashirika yote hayo manne yaliundwa ili kusaidia katika kufanikisha lengo maalumu la kueneza injili hasa katika nchi za misioni. Kazi yao kubwa ni kuongoza, kuratibisha, kuhamasisha na kuhimiza makanisa ya mahali (Local Churches) ili kutekeleza wajibu wa majukumu yao ya kimisionari.

Kwani kama Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani ulivyobainisha, “Kanisa zima ni la Kimisionari” Hali kadhalika kila muumini anapaswa kuwa na moyo wa kimisionari. Ndiyo kusema, inampasa kujitahidi kuzielewa vema kazi za misioni, kusaidia shughuli za umisionari kwa sala, sadaka na michango ya hali a mali ili kuufikisha Ufalme wa Mungu kwa mataifa yote ya ulimwengu. Kwa nia hiyo, maaskofu na mapadre katika nchi za misioni wanawezeshwa kusimika kanisa katika mataifa yote.

Mashirika hayo ambayo yemeenea katika makanisa karibu yote ulimwenguni yanayo makao makuu huko Roma; yakiongozwa na Halmashauri kuu (Superioir Council).

Historia ya Shirika

Awali, Shirika la Mtoto Yesu lilikuwa ni sehemu tu ya Shirika la Uenezaji Injili au Uenezaji Imani. Lakini kadri lilivyoenea na kukomaa, lilipata hadhi ya kuwa Shirika kamili lenye kujitegemea kwa kiasi fulani (With certain autonomy).

Mnamo mwaka 1842, Paulina Jaricot Yule mama mwanzilishi wa Shirika la kueneza imani alimweleza Askofu Forbin-Jonson wa Nancy (Ufaransa) maoni yake kwamba ingefaa kuanzisha chama cha pekee kwa ajili ya watoto wakatoliki ili kuwajengea moyo wa kimisionari tangu udogo wao kwa kujali shida na mahitaji ya watoto wenzao katika nchi za misioni- wafikirie njia ya kuwasaidia hao watoto maskini.

Askofu Forbin-Jonson alitambua mara moja umuhimu wa chama cha namna hiyo. Ndiyo chama hicho kikaundwa na kikaanza kuenea kwanza katika miji ya Ufaransa. Pole pole kilienea pi akatika nchi nyingine, na hatimaye Baba Mtakatifu alikitambua, akakipokea na kukipatia hadhi ya kuwa Shirika la Kipapa na kuhimiza lienezwe kote katika Kanisa Katoliki.

Tangu miaka michache baada ya kumaliziki kwa mtaguso mkuu wa pili wa vatikani, Maaskofu Katoliki nchini Tanzania waliamua kuwa shirika hilo lianzishwe pia hapa nchini kwetu.

Wakati shirika hilo lilipoanzishwa huko Ufaransa, tatizo kubwa lililoonekana kuzikabili nchi za misioni lilikuwa ni idadi kubwa ya watoto (hasa katika nchi ya India) walioachwa yatima ama kwa kufiwa na wazazi au kwa kutupwa. Kwa hiyo Paulina Jaricot alitamani kuwapatia wamisionari misaada ya sala na fedha ili kuwawezesha kuwapokea angalau baadhi ya watoto yatima, kuwapa makazi na chakula na kuwalea katika imani katoliki.

Uanachama

Shirika la Mtoto Yesu ni hasa kwa ajili ya watoto. Lakini hii haimaanishi kwamba haliwahusu watu wazima pia. Wao pia wanaweza kujishirikisha nalo. Masharti ya kuwa mwanashirika ni hasa mawili ambayo, kwa kweli ni rahisi sana:

  • Sala na Sadaka- Wanashirika wasali kila siku sala ya Salamu Maria na kuongeza maombi: “Bikira Maria Mtakatifu, utuombee sisi na watoto wote maskini na wenye shida popote ulimwenguni.”