INUKA CBR

ELIMU KUHUSU KITUO CHA UTENGAMAVU WA VIUNGO: INUKA CBR


UTANGULIZI

INUKA CBR ni kituo cha kiafya kinachohusika na huduma ya Utengamavu wa viungo kwa watu: watoto na watu wazima wenye shida ya ulemavu. Ni kituo kinachomilikiwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe kwa ushirikiano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Gondwana, Cesc Project, COMsol ya nchini Italia.

Lengo la INUKA CBR ni kuendeleza vipawa na kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kushirikiana na familia zao na jamii kwa ujumla. INUKA CBR ni kituo cha kijamii katika huduma hiyo ya utengamavu, INUKA CBR pia hutoa huduma ya vifaa saidizi mfano viungo bandia.

 1. MATATIZO YANAYOHUDUMIWA
 2. Tatizo La Miguu Rungu (Nyayo Zilizopinda)

INUKA CBR inawatibu watoto wenye umri chini ya miaka 5 ambao wamepata matatizo ya kupinda nyayo. Watoto hawa wanatibiwa kwa njia iitwayo PONSETI. Matibabu yao yana hatua kuu tatu:

Miguu rungu

i.Kupanga mifupa ya miguu na kufunga kwa kutumia P.O.P

ii.Operesheni ya misuli ya nyuma ya miguu

iii.Viatu maalum

 1. Mtindio Wa Ubongo

Mtindio wa ubongo ni tatizo linalotokana na kuumia ubongo wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.Tatizo hili hupelekea  misuli kulegea au kukakamaa na husababisha  mtoto kuchelewa katika hatua za ukuaji. Mfano kukaza shingo, kukaa, kutambaa, kusimama, na kutembea, udumavu wa akili, matatizo ya macho, dege-dege, na matatizo ya kuongea.

 1. Udumavu Wa Akili

Ni hali ambayo uwezo wa kiakili wa mtoto unakuwa chini ya kiwango cha kawaida.

 • Dalili Zake
 • Mtoto kushindwa kujifunza na kufanya shughuli za kila siku kama vile kuvaa na kuvua nguo, kwenda chooni, kunawa, kuoga, kupiga mswaki, kula, na shughuli nyingine za nyumbani.
 • Mtoto kushindwa kuchangamana na wengine: kuzubaa.
 1. Tatizo La Mtoto Kukosa Utulivu Na Umakini

Hili ni tatizo la mtoto kukosa umakini, kutokutulia na kufanya vitu bila mpangilio. Watoto hawa wanakuwa na uwezo mzuri wa kiakili na wanaweza kujifunza. Lakini tatizo la kutokutulia na kukosa umakini linawazuia kujifunza.

 1. Usonji

Ni tatizo ambalo mtoto anashindwa kuwasiliana, kuchangamana na anakuwa na tabia ya kufanya kitu kwa kujirudia rudia. Mfano kujipiga makofi, kung’ata ng’ata vidole na kujipigiza kichwa.

 1. Tatizo La Kichwa Kujaa Maji (Hydrocephalus) Na Mgongo Wazi

Matatizo haya hupelekea kuathirika kwa viungo vya mtoto aidha misuli kulegea na kukosa nguvu au kukakamaa na hivyo kusababisha mtoto kuchelewa katika hatua za ukuaji. Hii hutokana na presha ya mgandamizo kwenye mishipa ya fahamu kwenye ubongo au uti wa mgongo ambayo husababisha misuli kuathirika.

 1. Tatizo La Matege Kwa Watoto

Hili ni tatizo la kupinda miguu kwa watoto ambalo mara nyingi ni kawaida kwa watoto wengi na taratibu tatizo hili hujirekebisha kadiri mtoto anavyozidi kukua (kuanzia miezi 18). Kama miguu haijanyooka mpaka miaka 3, kwa hakika inawezekana kuna sababu inayofanya miguu kupinda. Miguu hupinda zaidi mtoto akianza kusimama na kutembea na anavyozidi kuongezeka uzito.

 1. Magonjwa Mbalimbali Ya Misuli

Baadhi ya magonjwa au matatizo husababisha mtoto kupooza misuli na kumfanya mtoto ashindwe kutumia viungo vyake katika shughuli mbalimbali. Mfano mtoto kuchomwa sindano vibaya au kuumia mishipa ya fahamu.

 1. Mongolia

Hili ni tatizo linalosababishwa na mabadiliko yasiyo ya kawaida yanayotokea kwenye vinasaba vya mtoto wakati wa ukuaji akiwa bado tumboni mwa mama. Hali hii hupelekea kubadilika kwa mtoto kimaumbile na kiakili. Mtoto anakuwa na mwonekano usio wa kawaida. Macho na masikio huwa madogo, uso wa mduara, kichwa kidogo, pua ndogo, kinywa kidogo na kutoa ulimi nje. Pia misuli yake huwa dhaifu na viungo laini, pamoja na udumavu wa akili. Kuchelewa katika hatua za ukuaji na baadae anakuwa na tabia ya kutokutulia.

 1. Tatizo La Miguu Kutokuwa Na Uvungu

Tatizo hili husababisha unyayo kupinda kwenda ndani na baadaye mtoto kupata maumivu jinsi anavyozidi kukua na kuongezeka uzito.

 1. Watoto Waliochelewa Katika Hatua Za Ukuaji

Tatizo hili husababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo ukosefu wa chakula bora au lishe bora (utapiamlo) na magonjwa mbalimbali.

 1. Watoto wenye matatizo ya kuongea

Katika hali ya kawaida mtoto anatakiwa aanze kutamka maneno mepesi akiwa na umri wa mwaka mmoja. Baada ya hapo ndani ya miaka miwili anatakiwa aanze kutengeneza sentensi nyepesi kama vile naomba, kula, na kadhalika. Kwa hiyo basi mtoto mwenye umri huo na bado hawezi kuongeea yafaa aletwe INUKA CBR kwa msaada zaidi.

 1. HUDUMA KWA WATU WAZIMA
 2. Tatizo La Kiharusi (Kupooza Upande Mmoja Wa Mwili)

Hili ni tatizo ambalo hutokana na sehemu ya ubongo kukosa damu ya kutosha au mishipa ya damu ya kwenye ubongo kupasuka  na damu kuvuja kisha damu kuganda kwenye ubongo kutokana  na mishipa hiyo kushindwa kuhimili presha kubwa. Hivyo hupelekea mtu kupooza upande mmoja wa mwili.

 1. Tatizo La Kuvunjika Uti Wa Mgongo

Tatizo hili linaweza kusababishwa na ajali au magonjwa yanayoshambulia uti wa mgongo na husababisha kupooza sehemu ya mwili. Inaweza kuwa miguu au mwili mzima.

 1. Maumivu Ya Mgongo

Maumivu chini ya mgongo, katikati au juu ya mgongo.

 1. Wagonjwa Waliokatwa Miguu

Tatizo linaweza kutokana na kupata ajali, athari za kisukari, kansa au sababu zingine. Kwa hiyo, tunatengeneza viungo bandia.

 1. Wagonjwa Waliopooza Viungo

Kupooza hutokana na sababu mbalimbali. Huku ni kupooza kwa mwili mzima au baadhi ya viungo vya mwili.

 1. Wagonjwa Wenye Shida Kwenye Joints (viungo mbalimbali vya mwili)

Mfano kushindwa kunyoosha au kukunja goti kutokana na athari za upasuaji, baada ya kuvunjika mfupa au kuumia kwenye kiungo  cha mwili.

Pia tatizo la Baridi Yabisi (maumivu kwenye joints kubwa za mwili mfano shingo, kiuno, mabega, mogoti, vifundo vya miguu).

 1. VIFAA VISAIDIZI

INUKA CBR inahusika pia na kutoa huduma ya vifaa saidizi kama vile viungo bandia vya miguu na mikono. Vifaa hivi ni kama vile vifaa vya mbao ,vitimwendo (wheel chair), viti maalum vya chooni, kigari cha kujifunzia kutembea na kadhalika.

 1. HUDUMA NYINGINE ZITOLEWAZO HAPA INUKA CBR

INUKA CBR pia inajihusisha na elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemavu, ushauri nasihi, pamoja na mafunzo na uhamasishaji kwenye jamii.

 1. UTARATIBU WA HUDUMA

INUKA CBR katika Kliniki ya mguu rungu, inatoa huduma hiyo kila Jumatano ya wiki ya huduma. Katika kila mwezi wiki ya kwanza hadi ya tatu ya mwezi ni wiki ya huduma kituoni (WIT). Na wiki ya nne au ya mwisho kila mwezi ni wiki ya huduma za utengamavu  majumbani.

 1. GHARAMA
 • Kufungua file na uchunguzi ni Tsh. 5,000/=
 • Wiki maalum ya huduma ya utengamavu ni Tsh. 15,000/= kila wiki kwa watoto
 • Mazoezi tiba: kwa watu wazima: Tsh. 4,000/= kwa kipindi kimoja cha dakika 45-saa 1 mara 2 kwa siku.
 • Mazoezi ya “gym”: Haya ni mazoezi yatolewayo kwa vijana mpaka watu wazima kwa ajili ya afya zao. Na gharama yake ni Tsh 1,000/=, hufanyika mara moja kwa siku na kwa saa moja kuanzia saa 11 hadi saa 12 jioni.
 • Hosteli: Vyumba vya kawaida, elfu nne (Tsh. 4,000/=) kwa chumba chenye vitanda viwili na elfu mbili (Tsh. 2000/=) kwa chumba chenye kitanda kimoja. Pia kwa chumba cha “self” ni elfu nane (Tsh. 8,000/=) kwa siku.
 • Ushauri nasihi kwa watu wazima wenye matatizo mbalimbali ya kisaikolojia, Tsh. 4,000/=
 • Kwa wale walio na ufadhili rasmi au wapo kwa usimamizi wa makampuni na mashirika rasmi wao wanachangia huduma kwa Tsh. 70,000/=

Ndugu zangu, hizo ni huduma ambazo zinapatikana INUKA CBR. Kama si wewe, basi ni jirani yako au ndugu yako au shangazi yako au mjomba wako hata shemeji yako anasumbuliwa na tatizo hilo. Hivyo, basi ni vema tusaidiane kwa kueneza huduma hii katika jamii zetu tupate kuisaidia kwa pamoja. Ahsanteni sana.

Kwa mawasiliano piga namba:

 1. Namba ya Kituo Mapokezi: +255(0)759750497
 2. Hussein Said (mtaalamu wa tiba viungo) +255(0)768718273
 3. Kaluwa Yohannes +255(0)765327912