Historia

Historia Fupi ya Jimbo la Njombe

Jimbo Katoliki la Njombe lilitangazwa rasmi tarehe 16 Februari 1968 Baba Mtakatifu Paulo VI. Mheshimiwa Padre Bruno Zwissler OSB aliyekuwa Naibu wa Askofu (Vicar General) kwa ajili ya parokia za Wilaya ya Njombe aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume (Apostolic Administrator) wa Jimbo jipya la Njombe. Makao makuu ya Jimbo la Njombe yakawa ni Njombe mjini.

Wakati wa kutangazwa, Jimbo lilikuwa na parokia kumi na tano (15) zilizoanzishwa na Wamisionari Wabenediktini na parokia sita (6) zilizoanzishwa na Wamisionari Wakonsolata na kufanya jumla ya parokia ishirini na moja (21) zenye wakristo 97,000. Tarehe 17.6.1968 Baba Askofu Eberhard Spies OSB wa Jimbo la Peramiho kwa niaba ya Baba Mtakatifu Paulo VI alimkabidhi Padre Bruno Zwissler rasmi Jimbo jipya la Njombe na kumsimika kama Mkuu wa Jimbo hilo mbele ya mapadre, watawa na walei wa jimbo lake katika Kanisa la Njombe Mjini.

Mheshimiwa Padre Bruno Zwissler OSB alimchagua Padre Bosco Brunner OSB kuwa Naibu wa Askofu (Vicar General) na Br. Folkward Gothe OSB alikuwa Mhasibu wa Jimbo katika miaka ya mwanzo takribani kwa miaka thelathini 30 hivi. Kama ilivyo kwa mtoto mchanga, katika kipindi cha mwanzo Jimbo lilipitia wakati mgumu na kuwa na matatizo mengi.

Mwaka 1970 Mheshimiwa Padre Raymond Mwanyika alichaguliwa kuwa Naibu Mkuu wa Jimbo la Njombe badala ya Padre Bosco Brunner OSB.

Katika kuweka misingi thabiti ya Jimbo, Padre Bruno Zwissler OSB aliwaunganisha wamisionari Wabenedicktini na Wakonsolata wafanye kazi kama timu moja katika Jimbo. Alianzisha Seminari ya Mafinga akishirikiana na Askofu Mario Mgulunde aliyekuwa askofu wa Jimbo la Iringa. Wakati wa uongozi wake wa miaka mitatu (1968-1971) zilianzishwa Parokia za Matamba (1968) na Kifumbe (1969).

Mnamo mwaka 1968 alianza kujenga nyumba ya Masista Wabenediktini wa Mtakatifu Agnes huko Imiliwaha karibu na Parokia ya Matola.

Tarehe 22 Februari 1971 Baba Mtakatifu Paulo VI alimteua Mheshimiwa Padre Raymond Mwanyika kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo la Njombe. Tarehe 25.04.1971 Mwadhama Laureano Kardinali Rugambwa alimweka wakfu Mhashamu Askofu Mteule Raymond Mwanyika mbele ya maaskofu wageni waalikwa na umati mkubwa wa wakristo wa jimbo lake. Sherehe za kufana zilimpokea Askofu Mwanyika katika jimbo lake.

Hayati Askofu Raymond Mwanyika alistaafu rasmi mwaka 2002 kutokana na shida ya afya. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua Padre Alfred Leonhard Maluma kuwa Askofu wa pili wa Jimbo la Njombe Juni 2002. Askofu Mteule Alfred Maluma aliwekwa wakfu na kusimikwa rasmi na Mwadhama Polcarp Kardinali Pengo Septemba 1, 2002 Katika viwanja vya Kanisa Kuu la Jimbo la Njombe. Kwa sasa (wakristu, mapadre, watawa, eneo, parokia idadi)

Historia Ndefu

Mahali Lilipo

Jimbo Katoliki Njombe limo katika Mkoa wa Njombe, Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania, kati ya nyuzi za Longitudo 33055’ na 35045’ mashariki na Latitudo 8050’ na 10030’ kusini. Jimbo la Njombe linapakana na majimbo mengine Katoliki yafuatayo: Mashariki-Jimbo la Mahenge, Magharibi-Jimbo la Mbeya, Kaskazini-Jimbo la Iringa, Kusini-Jimbo Kuu la Songea na Jimbo la Mbinga.

Eneo na Idadi ya Watu

Jimbo la Njombe linajumuisha na kuunganisha wilaya nne za Mkoa wa Njombe ambazo ni Njombe, Ludewa, Makete na Wanging’ombe ambazo zina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 24 994.

Jimbo linakadiriwa kuwa na wakazi 719 151 (Regional NBS) kwa mujibu wa sensa ya wakristo ya mwaka 2015 iliyofanywa na Jimbo la Njombe.

Waamini Wakatoliki: 265146 Wakatekumeni: 8 498 Waprotestanti: ca 254005 Wasio Wakristo: ca 200 000 Wasio Wakatoliki: ca 454005

Sura na Tabia ya Nchi

Jimbo la Njombe lina kanda za joto na kanda za baridi. Pia kuna sehemu chache zenye hali ya vuguvugu kufuatana na mwinuko wa ardhi kutoka usawa wa bahari. Sehemu za kusini za Jimbo kando kando ya Ziwa Nyasa wastani wa joto ni nyuzi 250C katika mwaka; lakini sehemu za magharibi za jimbo (wilaya ya Makete na sehemu ya wilaya ya Wanging’ombe( wastani wa joto ni nyuzi 100C. Sehemu kubwa ya jimbo iliyobaki ina wastani wa nyuzi joto 150C na 200C. Vilevile zipo sehemu chache jimboni ambazo hupata joto chini ya nyuzi 50C wakati wa kipindi cha baridi miezi ya Juni na Julai.

Mwinuko wa ardhi Jimboni ni kati ya mita 500 na 2500 kutoka usawa wa bahari kwa wastani na milima ya Kipengere inakaribia mita 3000 kutoka usawa wa bahari. Jimbo la Njombe lina sehemu zenye milima yenye mitermko mikali kwa mfano Milima ya Livingstone, Kipengere na Matamba. Vilevile zipo sehemu chache zenye mabonde makubwa katika wilaya za Makete na Ludewa. Sehemu kubwa ya Jimbo ni mbuga zenye mwinuko wa wastani, hasa katika wilaya za Njombe na Wanging’ombe.

Njombe ina misimu miwili katika mwaka: msimu wa mvua (Novemba-April) na msimu wa kiangazi (Mei-Oktoba). Sehemu nyingi za Njombe hupata mvua za wastani wa milimita 1600 kwa mwaka.

Historia ya Jimbo

Kanisa Katoliki liliingia Njombe baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia 1914-1918. Serikali ya Kijerumani iliweka mipaka ya madhehebu ya Kikatoliki na Kilutheri katika ukanda wa Kusini-Magharibi mwa Tanganyika kabla ya vita kuu. Kusini mwa Mto Ruhuhu na Mto Lukumburu ilikuwa ni eneo la Kanisa Katoliki, na Kaskazini mwa mito hiyo hadi Ruaha, Usangu na Kufuata milima ya Udzungwa ilikuwa ni eneo la Kanisa la Kilutheri. Mwaka 1924 Padre Gallus Steiger OSB akiwa msimamizi wa Jimbo la Lindi (Perfectura) katika kikao na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Songea alikataa kuiwekea mipaka Injili ya Kristo. Mkuu huyo wa wilaya alipeleka swala la mipaka kwa wakuu wake huko Dar es Salaam. Gavana wa Dar es Salaam alishindwa kulitatua suala hili, ndipo yeye na halmashauri yake walilipeleka London-Uingereza kwa Katibu wa Makoloni. Katibu huyo alilipeleka swala la mipaka Umoja wa Mataifa (League of Nations) huko New York Marekani.

Jibu kutoka huko lilikuwa kwamba katika nchi za makoloni Dini ni Uhuru. Jibu hilo lilitumwa kwa simu (Telegraph) kwa wahusika mpaka Songea. Kutokana na majibu mazuri ya simu kutoka Umoja wa Mataifa Padre Hilari Kaiser OSB wa Missioni ya Lituhi alivuka mto na kuingia Upangwa na pia Padre Xaver Hassler wa Missioni ya Peramiho aliwatuma makatekista Mahanje. Makatekista hawa walivuka Mto Ruhuhu wakafika kwa Jumbe Msambichaka. Makatekista wengine walifika Lukumburu, wakafika kwa Mafutagang’ombe Njalika wa Ihanga. Wengine walifika hata kwa Jumbe Matola Mdendemi. Mwaka 1926 Padre Joseph Damm alifika Lituhi. Kutoka Lituhi alianzisha Parokia ya Lugarawa 1928. Mwaka 1931 alianzisha Parokia ya Uwemba. Padre Thadei OSB alianzisha Parokia ya Lupingu mwaka 1932, Padre Oswald OSB alianzisha Missioni ya Mahanje 1926 na akatembelea sehemu za Ubena walikotumwa makatekista wa kwanza mpaka kwa Mafutagang’ombe sasa Ihanga.

Mwaka 1933 Wamisionari Wakonsolata toka Tosamaganga waliingia Njombe Kaskazini. Padre Guido Bartorellli alianzisha Missioni ya Kipengere 1933. Missioni ya Matembwe nayo ikaanzishwa mwaka huo huo 1933. Wamisionari wa mashirika haya mawili Wabenediktini na Wakonsolata walieneza Kanisa Katoliki katika Wilaya ya Njombe kwa mafanikio ya kuridhisha kama alivyotabiri Askofu Gallus Steiger OSB. Yeye aliwaambia Makatekista aliokuwa anawatuma kwenda Ubena: “Salini sana kwa Mama Bikira Maria Imakulata atusaidie tuipate ile nchi ya Ubena, kwani ninona kule itazaliwa miito mingi sana, na kutakuwa na wakristo wengi na hodari.” Maneno haya aliyasema Katekista Gabriel Komba wa Mgazini aliyetumwa Wino mwaka 1923.

Kuzaliwa Jimbo la Njombe

Misioni za Wilaya ya Njombe pamoja na Mahanje na Ifinga ziliwekwa katika kundi moja zikiitwa Kanisa Katoliki la Kaskazini. Wamisionari wa eneo hili walifanya mikutano yao pamoja. Wazo la kuanzisha jimbo katoka eneo la Njombe lilikuwamo katika fikra za wamisionari tangu muda mrefu. Ilifika wakati kazi ya Kanisa ya kuhubiri Injili ilikuwa imepanuka sana. Ukubwa wa Jimbo la Peramiho na mahitaji ya kichungaji yalikuwa ni sababu kubwa ya kugawa Jimbo la Peramiho. Wilaya ya Njombe ilikuwa na Naibu wa Mhashamu Askofu Eberhard Spiess OSB wa Peramiho aliazimia kuligawa Jimbo la Peramiho. Alimwomba Baba Mtakatifu Pius XII naye akamwidhinisha. Tarehe 16 Februari 1968 ni siku ya kihistoria kwani Baba Mtakatifu Paulo VI alitangaza rasmi Jimbo jipya la Njombe na mheshimiwa Padre Bruno Zwissler OSB aliyekuwa Naibu wa Askofu (Vicar General) kwa ajili ya parokia za Wilaya ya Njombe aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume (Apostolic Administrator) wa Jimbo jipya la Njombe. Makao makuu ya Jimbo la Njombe yakawa ni Njombe mjini.

Jimbo hili jipya lilikuwa na parokia kumi na tano (15) zilizoanzishwa na Wamisionari Wabenediktini na parokia sita (6) zilizoanzishwa na Wamisionari Wakonsolata. Jumla zilikuwa parokia ishirini na moja (21) zenye wakristo 97,000. Tarehe 17.6.1968 Baba Askofu Eberhard Spies OSB wa Jimbo la Peramiho kwa niaba ya Baba Mtakatifu Paulo VI alimkabidhi Padre Bruno Zwissler rasmi Jimbo jipya la Njombe na kumsimika kama Mkuu wa Jimbo hilo mbele ya mapadre, watawa na walei wa jimbo lake katika Kanisa la Njombe Mjini.

Mheshimiwa Padre Bruno Zwissler OSB alimchagua Padre Bosco Brunner OSB kuwa Naibu wa Askofu (Vicar General) na Br. Folkward Gothe OSB alikuwa Mhasibu wa Jimbo katika miaka ya mwanzo takribani kwa miaka thelathini 30 hivi. Katika kipindi cha mwanzo Jimbo lilikuwa na matatizo ya kila aina kama motto mchanga.

Mwaka 1970 Mheshimiwa Padre Raymond Mwanyika alichaguliwa kuwa Naibu Mkuu wa Jimbo la Njombe badala ya Padre Bosco Brunner OSB. Mheshimiwa sana Mkuu wa Jimbo Padre Bruno Zwissler OSB alifanya kazi nzuri ya kuweka misingi thabiti ya jimbo lake. Aliwaunganisha wamisionari wa mashirika mawili wafanye kazi kama timu moja katika Jimbo. Alianzisha Seminari ya Mafinga akishirikiana na Mkuu wa Jimbo la Iringa Askofu Mario Mgulunde. Wakati wa uongozi wake wa miaka mitatu (1968-1971) zilianzishwa Parokia za Matamba (1968) na Kifumbe (1969). Alianza kujenga nyumba ya Masista Wabenediktini wa Mtakatifu Agnes huko Imiliwaha karibu na Parokia ya Matola (1968).

Tarehe 22 Februari 1971 Baba Mtakatifu Paulo VI alimteua Mheshimiwa Padre Raymond Mwanyika kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo la Njombe. Tarehe 25.04.1971 Mwadhama Laureano Kardinali Rugambwa alimweka wakfu Mhashamu Askofu Mteule Raymond Mwanyika mbele ya maaskofu wageni waalikwa na umati mkubwa wa wakristo wa jimbo lake. Sherehe za kufana zilimpokea Askofu Mwanyika katika jimbo lake.

Hayati Askofu Raymond Mwanyika alistaafu rasmi mwaka 2002 kutokana na shida ya afya. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua Padre Alfred Leonhard Maluma kuwa Askofu wa pili wa Jimbo la Njombe Juni 2002. Askofu Mteule Alfred Maluma aliwekwa wakfu na kusimikwa rasmi na Mwadhama Polcarp Kardinali Pengo Septemba 1,2002 Katika viwanja vya Kanisa Kuu la Jimbo la Njombe.

Kukua kwa Uchungaji

Wamisionari wa Mwanzo Jimboni Njombe

Wamisionari walioleta Injili katika Jimbo la Njombe walikuwa wa Mashirika mawili, yaani Wabenediktini na Wakonsolata.

Shirika la Wamisionari wa Mt. Benedikto

Shirika la Wamisionari wa Mtakatifu Benedikto (Wamisionari Wabenediktini) lilianzishwa na Padre Andreas Amhein 1884 huko St. Otilien-Ujerumani. Kwa mapendekezo ya Baron von Gravenreuth wa Kampuni ya German East Africa, wamisionari Wabenediktini waliombwa kuhubiri Injili Tanganyika kwa sababu walikuwa wa taifa lao. Wakati huo wamisionari wengi Tanganyika walikuwa Wafaransa. Roma iliwatuma Wabenediktini Afrika Mashariki Jimbo la Zanzibar Novemba 1887. Wabenediktini waliingia Dar es Salaam – Tanganyika kupitia Zanzibar mwezi Januari 1888. Tarehe 30.09.1894 Padre Maurus Hartman aliingia Lindi. Mwaka 1898 Askofu Cassian Spiss alianzisha Missioni ya Peramiho tarehe 22 Desemba 1931 Baba Mtakatifu Pius XI aliunda Abasia ya Ndanda na Peramiho. Mheshimiwa Padre Gallus Steiger OSB alikuwa Abate wa Kwanza wa Abasia ya Peramiho. Mwaka 1934 aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo la Peramiho. Kutoka Peramiho wamisionari wengi walitumwa pande zote za eneo la Abasia kuhubiri Neno la Mungu na kuanzisha misioni. Wamisionari mashuhuri wa mwanzoni walioleta Injili katika wilaya ya Njombe ni Padre Xaver Hassler OSB, Padre Joseph Damm OSB, Padre Oswald OSB wa Mahanje, Padre Elias OSB, Padre Meinulf OSB, Padre Thadei OSB na Padre Leonard OSB. Pamoja nao walikuwapo masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing waliofanya kazi za kuinjilisha katika misioni hizo hizo.

Shirika la Wamisionari Wakonsolata

Shirika hili la kimisionari lilianzishwa na Padre Yosef Allamano huko Torino-Italia 1901. Lengo lake kuu lilikuwa kuanzisha shirika la kimisionari haswa na si kwa maisha ya kitawa bali familia yenye moyo wa kueneza Neno la Mungu.

Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) Wajerumani walishindwa. Wamisionari Wabenediktini ambao walikuwa na asili ya Ujerumani walifukuzwa toka Tanganyika. Ili kazi ya umisionari iliyoanzishwa nao isiwe bure, Idara ya Uenezaji Injili ya Ofisi Kuu ya Baba Mtakatifu huko Vatikano (Propaganda Fide) iliwaomba Wamisionari Wakonsolata wafike Tanganyika kushika misioni zilizoachwa na Wabenediktini. Mwaka 1919 Wamisionari Wakonsolata walifika Tosamaganga, Madibira, Bihawana na Sanza. Wamisionari wa kwanza kama Padre Francesco Cagliero IMC, Padre Cavallo IMC, Padre Balbo IMC na wenzao walitokea Kenya. Mkubwa wao alikuwa Padre Cagliero IMC.

Haikuwa rahisi kwa Wamisionari Wakonsolata kuingia Njombe. Mipaka iliyowekwa na serikali ya Ujerumani na kukubalika na Balozi wa Baba Mtakatifu Mhashamu Askofu Hinsley iliwazuia Wakonsolata kujipenyeza Njombe. Katiba ya Umoja wa Mataifa (League of Nations) iliondoa mipaka hiyo. Baada ya mheshimiwa Padre Cagliero kuwekwa kuwa Mkuu wa Jimbo la Iringa, Wakonsolata walianza kuingia Njombe. Padre Alfred Ponti alikuwa mtangulizi kama Padre Maurus Hartmann alivyofanya kwa upande wa Wabenediktini.

Misioni za kwanza zilikuwa Kipengere na Matembwe. Misioni ya Matembwe ilianzishwa na Padre Nebbia 1933. Padre Nebbia alinunua shamba la ekari zaidi ya elfu moja toka kwa mzungu mlowezi Bwana Read kutoka Afrika ya Kusini. Padre Guido Bartorelli alinunua shamba la Kipengere na kuanza misioni mwaka 1933. Padre huyu alizunguka eneo la Ukinga kwa kuwa eneo hili likuwa limeshapokea dhehebu la Lutherani kabla ya 1900, kwa taabu na magomvi milanga ikafunguka, akafanikiwa kuanzisha vigango. Mwaka 1956 Padre Lumetti alifaulu kuanza Misioni ya Kisinga. Pamoja na mwenzake Padre P. A. Placucci walitembelea sehemu za Uwanji mpaka Ziwa Nyasa. Eneo la Lumbila lilikuwa sehemu ya Wamisionari Wakonsolata. Sababu ya shida ya usafiri na kwa kuwa Wabenediktini wa Lupingu walikuwa wana vyombo vya kusafiria ziwani, waliishika sehemu hiyo ya mwambao wa ziwa. Hatimaye waliijenga misoni ya Lumbila.

Wakonsolata waliendelea kueneza Neno la Mungu Ubena. Padre Gramaglia alianzisha Misioni ya Igwachanya mwaka 1962 katika eneo la Misioni ya Kipengere. Misioni ya Matembwe ilihudumia eneo la Makambako na Kifumbe. Padre Barghetto alianzisha Misioni ya Makambako hapo mwaka 1954. Padre Cattoi alibaki Matembwe baada ya kuondoka Padre Nebbia. Padre Rigamonti alipokea Misioni ya Kipengere.

Parokia ya Ikonda na Matamba zilikuwa vigango vya Kisinga wakati wa Padre Lumetti. Padre Chiuch alianzisha Parokia ya Kifumbe mwaka 1969. Padre Daniel Armani alifungua Parokia ya Matamba mwaka 1968. Pamoja na hawa wamisionari mabradha na masista wa shirika hilo walitumwa pia kuinjilisha eneo la Njombe.

Shirika la Masista Wakonsolata lilianzishwa Torino-Italia na mwanzilishi yule yule Padre Allamano mwaka 1911 miaka kumi baada ya kuanzisha Shirika la mapadre na mabradha. Kazi za wamisionari hawa zimezaa matunda mengi na hasa kwa msukumo wa Askofu Beltramino, Neno la Mungu lilihubiriwa katika eneo la Njombe Kaskazini.