KONGAMANO LA MAKATEKISTA JIMBO

KONGAMANO LA MAKATEKISTA JIMBO LA NJOMBE

MAKATEKISTA! – UINJILISHAJI KWANZA!!!
Limefanyika kongamano kubwa la Makatekista Jimboni Njombe ambalo limekusanya makatekista 500 toka parokia zote 47 za Jimbo Katoliki la Njombe tangu 02-07-2018 na kuhitimisha tarehe 05-07-2018. Kongamano hili linatekeleza azimio la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambao waliagiza kila kundi katika Kanisa liadhimishe Jubilei ya miaka 150 kwa siku na vipindi maalum.

Makatekista wamejitokeza kwa wingi na kwa moyo wote kiasi kwamba hakuachwa katekista yoyote kigangoni kwake. Naye mkurugenzi wa Idara ya Katekesi Jimbo la Njombe Fr. Bruno Henjewele amewashukuru makatekista kwa mwitiko wao mkubwa katika utekelezaji wa kongamano hili. Katika kongamano hili makatekista wamejifunza mambo kadha wa kadha:
 Utume wa katekista hauna kikomo wala mipaka
o Yesu Kristo-ndiye kielelezo cha ukatekista na umisionari.
o Mtume Paulo – Katekista wa mataifa
o Wamisionari – kielelezo cha ufundishaji wa katekesi
 Utume wa Katekista na Katekisimu ya Kanisa Katoliki
o Katekista awe na ufahamu wa kutosha wa mafundisho ya Kanisa kadiri yalivyoandikwa kwenye Katekisimu.
o Katekisimu ni zana muhimu na ya msingi ya kufundishia mafundisho ya dini. Katekisimu inatupa msingi wa mafundisho ya imani yetu. Bila Katekismu utume wa Katekista hauna maana.
 Historia ya Kanisa miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara
o Wamisionari walituletea imani na kutukabidhi tuendelee wenyewe. Yatupasa kutafakari tumetoka wapi? Tupo wapi? Tunakwenda wapi?
Baada ya tafakari hiyo hatuna budi kutazama nini tumefanya na nini hatujafanya?
Kazi kubwa ya katekista sasa ni kusimamia na kutetea imani hii kama walivyoturithisha wamisionari wetu. Sasa ni zamu yetu. Kanisa lisifie mikononi mwetu.
o Imani ya Kanisa Katoliki na vikundi mbalimbali ndani ya Kanisa.

Makatekista mnahimizwa kuvilea vyama vya kitume katika vigango vyenu. Tupokee na kuvilea vyama halali vya kitume.
 Ujasiriamali, uchumi na fedha
o Katekista ni lazima ajishughulishe na ujasiriamali kwa namna moja au nyingine.
o Katekista uwe ni mfano wa kuigwa pale kigangoni ili na waamini waweze kuiga.
o Usipofanya kazi utakufa masikini.
o Ujasiriamali wa sasa unahitaji mpango mkakati – si kufanya tu kazi bila kuwa na malengo/mkakati maalum.
Ujasiriamali usio na mpango mkakati ni sawa na gari lisilokuwa na dereva.
Aidha makatekista waliofika kwenye kongamano walipata muda wa kujadiliana na kubadilishana mawazo na mbinu za uchungaji kutokana na changamoto zinazowakumba katika uchungaji wao.

Fr. Innocent Chaula