JUBILEI YA MIAKA 25 YA UPADRE

Furaha na shangwe zilitawala Kanisa Kuu la Jimbo la Njombe mnamo tarehe 11/10/2017 ambapo Jimbo lilifunga rasmi Mwaka wa Jubilei ya Upadre na pia kumshukuru Mungu kwa zawadi ya mapadre wane (4) waliosherekea Jubilei ya Miaka Ishirini na tano (25) ya Upadre ambao ni: Fr. Albert Mligo, Fr. Eventius Mdendemi, Fr. Gilbert Msaudzi na Fr. Paulinus Mligo
Jubilei hii ilifanyika tarehe hiyo ya 11 Oktoba kwa sababu maalum. Siku hii ndiyo aliyopadirishwa padre wa kwanza mzalendo jimboni Njombe hayati Padre Alois Kayombo. Aidha jubilei hii ilitanguliwa na mfungo kwa wajubilanti ambao wajubilanti hawa pamoja na mapadre wazee wengine katika jimbo ambao walikwisha kutimiza miaka ishirini na tano huko nyuma. Mapadre wazee walifika kwenye mfungo na kufanya mfungo pamoja na wajubilanti wa mwaka huu kwa lengo la kuamsha na kukumbushana fadhila na wajibu mbalimbali za kipadre. Pia walikuwa wanawapokea wenzao katika rika la uzee.
Misa Takatifu siku ya Jubilei ilitanguliwa na ibada ya mwanga ambapo Mhashamu Baba Askofu Alfred Maluma wa Jimbo la Njombe aliwasha mshumaa wa jubilei na kuwagawia mwanga huo (kuwawashia mishumaa) wajubilanti na kuongoza maandamano kuelekea kanisani. Misa ilihudhuriwa na mapadre, watawa na waumini wengi sana kutoka karibia kila parokia jimboni Njombe.
Katika mahubiri Mhashamu Askofu Maluma alisema: “Ndugu zangu mapadre, siku tulipopewa Daraja ya Upadre tulipakwa mafuta matakatifu kwa maneno yafuatayo: Bwana Yesu Kristo, ambaye Baba alimpaka mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu, akulinde kwa ajili ya kuwatakasa wakristo na kumtolea Mungu sadaka. Maneno haya yanatukumbusha kuwa padre ni mpakwa mafuta au mpakwa wa Bwana.
Mapadre wapendwa kumbukeni ile siku na dakika ile ulipopewa Daraja ya Upadre, ulipakwa mafuta matakatifu. Sasa mmetimiza miaka 25 na wengine zaidi. Mungu ametusaidia tumedumu mpaka hatua hii katika utumisha wa Bwana-katika ukuhani aliotushirikisha Yesu Kristo Kuhani Mkuu bila mastahili yetu. Kumbukeni na kuzingatia wajibu zenu za kipadre/kikuhani.
Waamini wapendwa leo tunasherekea Jubilei ya WAPAKWA WA BWANA pia miaka 100 iliyopita mapadre 6 wa kwanza walipatikana katika nchi yetu. Hawa walifungua mlango kwa neema za Mungu Tanzania imeendelea kuwapata wapakwa wengi mwaka kwa mwaka. Kwa njia ya mapadre Injili imehubiriwa, huduma ya masakramenti imezidi kutolewa, familia ya Mungu imehuishwa na kukua. Hivyo imekuwa hata katika jimbo letu kupitia utume wa mapadre wetu. Nawaalikeni nyote tuseme ASANTE MUNGU KWA MAKUU ULIYOTUTENDEA katika miaka hii ya utumishi wetu bila mastahili yetu. Kwenu wajubilanti AD MULTOS ANNOS!”
Aidha mara baada ya mahubiri wajubilanti pamoja na mapadre wote waliamsha viapo vyao vya upadre mbele ya Askofu wao wa Jimbo na mbele ya kanisa zima huku wakiwa wameshika mishumaa inayowaka.


Mwishoni mwa Misa Takatifu walipokea hati ya Baraka ya Kitume ya Jubilei kutoka kwa Baba Mtakatifu Francis.

Nadhiri na Jubilei ya Masista Wabenediktini-Imiliwaha

Jimbo la Njombe lilipata furaha kubwa pia ndani ya wiki moja kuwapata watawa waliofunga nadhiri zao za muda na za daima tarehe 17/10/2017. Mhashamu Askofu Maluma aliwakumbusha watawa hawa kuishi nadhiri zao za utii, ufukara na usafi wa moyo. Alisisitiza kuwa maisha ya utawa ni maisha ya sadaka lazima mtu ajitoe kweli kweli.
Siku iliyofuta yaani 18/10/2017 ilikuwa ni furaha kwa watawa wengine kufanya jubilei ya miaka Ishirini na tano ya nadhiri zao za kitawa. Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo la Mpanda aliongoza Misa hiyo na kuwakumbusha kuwa kutoka kwa mtawa kanisa linategemea kupata mtawa mwenye furaha, anayesali daima. Hata katika miaka ishirini na tano ya nadhiri bado mtawa aonekane mwenye furaha ya maisha ya kitawa. Yawapasa wajubilanti kutumia nafasi hii ya jubilei kama kituo cha mapumziko ili kukusanya nguvu za kuendelea mbele na safari ya maisha ya kitawa. Pia yawapasa kuwajali na kuwathamini watawa wenzao kwani pindi watakapokuwa wamechoka au kuishiwa nguvu ndio watakaowaisaidia kuwabeba au kuwakokota.